Tuesday , 9th Feb , 2016

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara Young African wanatarajia kuondoka hapo kesho alfajiri kuelekea nchini Mauritius kujiandaa na mchezo wa kwanza dhidi ya Cercle De Joachim huku ikiwaacha wachezaji wake watatu nchini.

Kocha Msaidizi wa Klabu hiyo Juma Mwambusi amesema mazoezi ya leo yamesaidia kuangalia hali ya wachezaji kwani jana kikosi kilipumzika baada ya mchezo wa Jumapili hivyo wachezaji ambao wataondoka nao watakuwa vizuri kwa ajili ya kuiwakilisha nchi.

Mwambusi amesema, mchezaji anaporejea kutoka majeruhi anakuwa taratibu katika mazoezi kama ilivyo kwa Nahodha wa Klabu hiyo Nadir Haroub Cannavaro ambaye ameshindwa kumaliza mazoezi pamoja na beki Haji Mwinyi ambaye amemaliza mazoezi mpaka mwisho lakini bado wanahitaji kumuangalia kwa siku ya kesho.

Mwambusi amesema, wanaamini watafanya vizuri katika mchezo wa awali japo mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na timu wanayokutana nayo kuwa na wachezaji wazuri hivyo hawawezi kuidharau timu yoyote watakayokutana nayo kwani kila timu imejipanga kwa ajili ya kupata mafanikio katika michuano hiyo.

Yanga inaondoka ikiwa na wachezaji wake 21 na viongozi saba ambapo itacheza mchezo wake wa kwanza jumamosi ya Februari 13 na kurudiana baada ya wiki mbili huku ikiwaacha mlinda mlango Benedict Tinoco, Mshambuliaji Geofrey Mwashiuya na mshambuliaji Matheo Anthony ambao pasi zao za kusafiria zinamatatizo.