Friday , 18th Sep , 2015

Wanamichezo wa hapa nchini waliokuwa wanachuana katika Michezo ya Africa wametoka mikono mitupu baada ya kufanya vibaya katika michezo mbalimbali waliyoshiriki katika fainali hizo zinazotarajiwa kumalizika kesho Jumamosi huko Kongo Brazaville.

Timu ya Tanzania iliwakilishwa katika michezo ya ngumi, riadha, judo, kuogelea, Paralimpiki (walemavu) na soka la wanawake.

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa BMT, Henry Lihaya, amesema wanariadha ambao walibakia wakipeperusha bendera ya nchi jana nao walishindwa kung'ara na kuifanya timu ya Tanzania kukosa medali ya aina yoyote.

Lihaya amesema, kati ya wanariadha wanne waliokimbia jana,Ally Khamis Gulam, ambaye aliingia hatua ya nusu fainali katika mita 200 naye hakufanya vizuri kwa kushindwa kupata nafasi ya kufika hatua ya fainali.

Lihaya amesema, changamoto kubwa waliyojifunza ni timu kutoka nchi nyingine kufanya maandalizi ya muda mrefu tofauti na wanamichezo wa Tanzania na uchache wa washiriki waliokwenda kushiriki michezo hiyo.