Wednesday , 11th Jun , 2014

Kamati ya rufani za uchaguzi ya TFF imetengua maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba ya kumuengua Michael Richard Wambura katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa klabu hiyo.

Michael Richard Wambura

Hatimaye uamuzi kuhusu rufani ya Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais wa klabu ya Simba umetangazwa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Uchaguzi ya TFF, Wakili Julius Lugaziya.

Wakili Lugaziya amesema kamati yake imefikia maamuzi ya kutengua maamuzi ya awali ya kamati ya uchaguzi ya Simba kwa kuwa klabu hiyo iliendelea kumshirikisha bwana Wambura na kumpatia majukumu na nyadhifa mbalimbali ndani ya klabu hiyo kama mwanachama hai licha ya kwamba alisimamishwa uanachama na kamati ya utendaji ya ya klabu hiyo tarehe 5 May 2010. Kitendo cha kumsimamisha halafu kumshirikisha katika mambo ya klabu ni sawa na kuyavunja maamuzi ya awali.

Aidha, Wakili Lugaziya amesema uamuzi wa kamati yake ambao ulifikiwa kwa upigaji wa kura kwa wajumbe kwa kuwa walishindwa kukubaliana kwa kauli moja, umezingatia busara zaidi ili kuiepusha Simba na migogoro isiyo ya lazima kwani endapo wangesimamia maamuzi ya awali ya kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo iliyo chini ya mwanasheria Damas Ndumbaro ambayo ilimuengua Wambura kwa kuwa uanacham a wake ni batili, basi mambo mengi ya klabu hiyo ambayo Wambura alishiriki kuyaandaa nayo yangekuwa batili ikiwemo kamati ya uchaguzi.

Baada ya kutenguliwa kwa maamuzi ya awali ya kamati ya uchaguzi, tulimtafuta bwana Wambura mwenyewe ili kujua alivyopokea maamuzi hayo. Katika mahojiano mafupi tuliyofanya naye, bwana Wambura amesema, "mpira ni mchezo wa mechi mbili...unacheza mechi ya kwanza ugenini halafu unacheza nyingine nyumbani. Hivyo ukijipanga unaweza ukautumia vizuri uwanja wa nyumbani"

Bwana Wambura alimalizia kwa kusema kwamba atafanya mkutano wa waandishi wa habari hapo kesho majira ya sita mchana, ili ayazungumzie kwa kina mambo anayoona ni ya muhimu wanasimba kuyajua.