Wednesday , 29th Jun , 2016

Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Mara Michael Wambura amesema ameanzisha mkakati kabambe utakaoufanya mkoa huo unaingia katika ramani ya soka hapa nchini.

Michael Wambura akizungumza na EATV.

Wambura ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF amesema mara baada ya kushinda katika uchaguzi wa chama, amebaini changamoto nyingi zinazowakabili ambazo anaamini kwa umoja watakaokua nao watapeleka timu ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Ameongeza kuwa kwa sasa watahakikisha wanaimarisha vyama vya soka katika kila ngazi ya mkoa hadi wilaya lakini pia wanapambana ili kurejesha imani kwa wadau wa michezo wakiwemo wadhamini ambao kwa kiasi kikubwa walijitoa kusapoti mpira kutokana na mizengwe iliyokua imeshamiri.

Hata hivyo Wambura amesema mikakati hiyo si ya mtu mmoja bali ni ya wadau wote wa mkoa wa Mara ambao endapo wataamua watauletea heshima mji wao kupitia michezo.

Wambura anakumbukwa kwa changamoto alizokutana nazo kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi mbali mbali mara sita, ikiwemo pia kufungiwa kujihusisha na masuala ya soka haswa enzi za aliyekua raisi wa TFF Leodgar Tenga akidaiwa kukiuka maadili.