
Timu za soka za wanawake nchini zikichuana katika ligi hiyo hatua za awali.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema hii leo kwamba kutoka Kundi B timu zote tatu za kusonga sita bora zimekamilika mbazo ni JKT Queens ya Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwani na Fair Play ya Tanga.
Timu zilizokosa nafasi ya kusonga mbele kutoka kundi hilo ni Evegreen ya Temeke, Mburahati Queens ya Dar es Salaam na Viva ya Mtwara.
Lucas amesema timu zilizofuzu hadi sasa kutoka Kundi A ni Sisters ya Kigoma na Marsh Academy ya Mwanza.
Timu nyingine zilizobaki ambazo zinawania nafasi moja ya kukamilisha timu za kufuzu Sita Bora kutoka kundi hilo ni Panama ya Iringa, Baobab ya Dodoma, Majengo ya Singida na Victoria na Queens ya Kagera.
Hatua ya Sita Bora inatarajiwa kuanza katikati ya mwezi katika uwanja wa Karume, Dar es Salaam na bingwa atajainyakulia Kombe na Medali za Dhahabu, mshindi wa pili Kombe na Medali za Fedha.