Sunday , 16th Sep , 2018

Wanariadha wa Kenya wameendelea kufanya vizuri kwenye ramani ya mchezo huo duniani, baada ya leo mwanariadha Eliud Kipchoge kuvunja rekodi ya dunia kwenye mbio za Berlin Marathon.

Gladys Cherono na Eliud Kipchoge

Katika mbio hizo kubwa na zenye heshima duniani zilizofanyika leo Kipchoge, ametumia saa 2:01:39 kukimbia kilomita 42.195 hivyo kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Mkenya mwingine Dennis Kimetto ambaye alitumia saa 2:02:57 mwaka 2014.

Kwa upande wa wanawake mwanariadha Gladys Cherono wa Kenya ameshinda baada ya kutumia saa 2:18:11. Cherono sasa anakuwa mwanariadha wa 4 duniani kwa upande wanawake kutumia muda mfupi zaidi kumaliza mbio hizo.

Kipchoge anatajwa kama mwanariadha bora zaidi kuwahi kutokea kutoka na mafanikio yake ambapo mapema mwaka huu alishinda mbio za London Marathon kwa mara ya tatu huku pia akiwa ni bingwa wa olimpiki wa mbio ndefu.

Katika mbio za leo kwa wanaume, Kenya imefanikiwa kuchukua nafasi zote tatu za juu ambapo wanariadha Amos Kipruto na Wilson Kipsang wameshika nafasi za pili na tatu. 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, amewapongeza wanariadha hao kwa ushindi wao.