Friday , 26th Jan , 2018

Kuelekea mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara raundi ya 15 kati ya Azam FC dhidi ya Yanga, klabu ya Azam imeomba kubadilishwa kwa mwamuzi wa kati aliyepangwa na bodi ya ligi kuchezesha pambano hilo.

Mwamuzi ambaye amepangwa kuchezesha mchezo huo wa jumamosi ni Israel Nkongo, ambaye Azam FC imeijulisha bodi ya ligi kuwa mwamuzi huyo amekuwa na mapungufu mengi kwenye uchezeshaji hivyo hawana imani naye.

Azam FC pia wamesema moja ya sababu kubwa ambazo zimepelekea wao kuomba kubadilishiwa mwamuzi ni maamuzi ya Nkongo kwenye mechi ya ligi kuu aliyochezesha wiki moja iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kuzua utata mkubwa.

Ombi hilo la Azam FC limewasilishwa kwenye bodi ya ligi, Kamati ya waamuzi na klabu ya Yanga ambayo ndiyo watacheza nayo. Mwaka 2016 nchini Hispania mwamuzi msaidizi kwenye mechi ya Elclasco alifungiwa wiki mbili baada ya kuonekana kuwa karibu na wachezaji wa Barcelona.

Waamuzi wengine waliopangwa kushirikiana na Nkongo kwenye mechi hiyo ni Josephat Bulali msaidizi namba moja, msaidizi namba mbili Soud Lila, mwamuzi wa akiba ni Elly Sasii na kamishna ni Omar Abdulkadir wote wakitoka Dar es Salaam.