Monday , 30th Mar , 2015

Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga amesema Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA, Sepp Blatter amepewa nafasi na viongozi wa Soka Barani Afrika katika kushinda Uchaguzi Mkuu wa FIFA.

Tenga amesema, viongozi wa Soka Afrika waliokutana Juni mwaka jana katika Mkutano Mkuu wa Viongozi wa Afrika uliofanyika Sao Paulo nchini Brazil walikubali kumuunga Mkono Blatter kutokana na msimamo wake usiotetereka wa kusaidia maendeleo ya mpira katika nchi changa ikiwemo Afrika.

Tenga amesema, Dunia ya Mpira ni siasa na Afrika mambo yake mengi yamefanikiwa ndani ya FIFA kutokana na Blatter kuwa pamoja na Afrika kusimamia yale wanayoyaona suala lililochangia viongozi wengi wa Afriika kutambua mchango wa Rais huyo katika Soka katika Bara la Afrika.

Tenga amesema huo umechukuliwa kama msimamo wa viongozi ambao wameuona na kuthibitisha mchango wa Blatter katika kukuza na kuendeleza Soka barani Afrika.

Blatter, mwenye Umri wa Miaka 78, anawania Urais kwa Mara ya 5 tangu atwae wadhifa huo Mwaka 1998 na anatarajiwa kushinda tena kwenye Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mei 29 Mwaka huu, Mjini Zurich huku akitegemewa kuzoa Kura toka Asia, Afrika na Marekani ya Kusini ambako ndiko waliko Wanachama wengi wa FIFA ukilinganisha na 53 wa Ulaya kati ya Wanachama 209 Dunia.