Monday , 30th May , 2016

Kuelekea katika mchezo wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars dhidi ya timu ya Taifa ya Misri, Kocha wa Stars Charles Mkwasa, amesema katika mchezo huo ushindi wa aina yoyote utasaidia kuweka heshima ya Tanzania katika soka.

Mkwasa amesema, wanahitaji matokeo mazuri hususani magoli manne au zaidi kwani italeta mabadiliko pia katika soka na kuweza kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Nigeria.

Mkwasa amesema, amejaribu kutafuta wachezaji wenye kiwango kizuri kwa sababu muda wa kujiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Misri ni mdogo hivyo wachezaji watakuwa wakijirekebisha kidogo kwa ajili ya mchezo huo.

Mkwasa amesema, anaamini watanzania kwa ujumla wataridhika na matokeo kwani kikosi kinaendelea kujiandaa kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itashuka dimbani Juni 04 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikwa ni mchezo wa marudiano dhidi ya Misri katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za AFCON 2017 nchini Gabon.

Baada ya mchezo dhidi ya Misri, Stars itacheza mechi ya mwisho na Nigeria Mjini Lagos Septemba mwaka huu. Katika mchezo wa awali uliochezwa nchini Misri hapo mwaka jana, Stars ilipoteza mchezo huo baada ya kuchapwa mabao 3-0. Nafasi ya Nigeria na Stars kufuzu imetoweka baada ya kujitoa kwa Chad kwenye kundi G.

Misri wanaendelea kuwa kileleni mwa Kundi wakifuatiwa na Nigeria, huku mtihani ukibaki kwa Tanznaia yenye pointi moja ambayo inahitaji nafasi ya kushiriki AFCON 2017 Gabon, ila mchezo wake wa marudiano dhidi ya Nigeria Septemba 2 unatabiriwa kuwa utakuwa mgumu.