Friday , 3rd Mar , 2017

Uongozi wa klabu ya Yanga umeshikwa kigugumizi na kushindwa kuthibitisha iwapo ni mkurugenzi wake wa ufundi Hans van der Pluijm ameachana na klabu hiyo au lah..!!

Hans van der Pluijm

Taarifa za Hans kuachana na Yanga zimevuma na kuenea kwa kasi mchana wa leo, ambapo kuna taarifa kuwa mdachi huyo ambaye ndiye aliyekuwa kocha wa Yanga kabla ya kuajiriwa kwa George Lwandamina, mkataba wake umefikia ukomo na kwamba klabu haijawa tayari kumuongezea mkataba.

Akizungumza na EATV Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa amesema kuwa uongozi haupo kwenye nafasi ya kulizungumzia suala hilo kwa sasa hadi utakapomaliza mechi yao na Mtibwa Sugar, siku ya Jumapili wiki hii.

"Ufafanuzi ni kwamba sisi kwa sasa tuko busy na maandalizi ya kwenda Morogoro kwenye mchi na Mtibwa, hilo suala tutalizungumzia tutakapokuwa tumemaliza hiyo mechi, tutaitisha kikao, tutaweka wazi kuthibitisha yote hayo" Amesema Mkwasa

Boniface Mkwasa Katibu Mkuu wa Yanga

Kuhusu mkataba wake kumalizika, Mkwasa amesema kwa muda huu hakumbuki kama mkataba wake umeisha au vipi hadi atakapoangalia kwenye kumbukumbu zake.

"Mkataba wake mpaka niangalie kwenye records, sasa hivi siwezi kukumbuka, taarifa itatoka rasmi, ninaposema hivyo inamaana nathibitisha sasa kama hivyo, nisubiri nishughulikie masuala ya timu kwanza halafu ndiyo utaniambia hayo masuala ya mtu mmoja maana siwezi kuzungumzia suala la mtu mmoja wakati timu nataka niipeleke Morogoro kuna mechi Jumapili" Amemalizia Mkwasa.

Uchunguzi wa EATV umebaini kuwa Hans aliachana na klabu hiyo tangu juzi, Machi 01, mwaka huu, ingawa haijafahamika mara moja sababu ya kuachana huko