Wednesday , 10th Dec , 2014

Timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars imeanza mazoezi katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, ikiwa ni maandalizi ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza na East africa Radio, Kocha wa Timu hiyo, Rogasian Kaijage amesema mechi hiyo itakuwa ni majaribio kwa ajili ya maandalizi ya kufuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika inayotarajiwa kufanyika Machi mwakani ambapo programu ipo tayari na ameshaandaa timu.

Kaijage amesema wameanza mazoezi madogo madogo ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa wachezaji hao ambapo hawajaanza kambi rasmi lakini wanatarajia kuanza kambi rasmi mapema wiki ijayo.

Kaijage amesema kikosi hicho ni mchanganyiko wa wachezaji wa timu ya vijana pamoja na timu ya wakubwa aliyoiunda mwaka jana kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Kaijage amesema mchanganyiko wa wachezaji hao utasaidia kuweza kupata vijana ambao wataweza kufanya vizuri katika mashindano makubwa na kufika wanapopatarajia katika soka la wanawake hapa nchini.