Friday , 1st Feb , 2019

Klabu ya Namungo FC inayosapotiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa imesema kuwa haitishiki na ushindi wa Yanga katika mchezo wake katika kombe la shirikisho.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kikosi cha Yanga kikiwa mazoezini

Uongozi wa klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza kupitia kwa mwenyekiti wake, Hassan Zidadu umesema kuwa hauhofii kukutana na Yanga kwani wamejipanga kucheza na timu yoyote.

"Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wenye uwezo ila hilo halitupi mashaka kwani mpira ni mchezo wa makosa nasi tunaanza kujipanga ili tukikutana nao tuwe fiti kwelikweli", amesema.

"Hatuna mashaka na timu yoyote ambayo tutapambana nayo, kwa kuwa wameshinda basi wakaribie tu huku kwetu Lindi tuwaonyeshe namna ambavyo mpira unachezwa maana hatubahatishi na hatuna hofu", ameongeza Zidadu.

Kwa mujibu wa ratiba ilivyo, Februari 22 hadi 25,  Yanga baada ya kushinda dhidi ya Biashara United, itapambana na Namungo FC ya mkoani Lindi katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.

Namungo inaongoza kundi A ikiwa na pointi 23 imecheza michezo 11 kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Ikumbukwe timu hizi ziliwahi kukutana mwaka uliopita katika mechi ya kirafiki ya kuzindua uwanja wa klabu ya Namungo uliopo wilayani Ruangwa mkoani Lindi unaojulikana kwa jina la 'Majaliwa' na mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.