Wednesday , 22nd Apr , 2015

Shirikisho la Ngumi Nchini BFT, limesema timu ya taifa ya ngumi ya wanaume imepata mualiko kutoka nchini Zambia kwa ajili ya mapambano ya kirafiki yatakayofanyika Mei mwaka huu ambapo kutakuwa na nchi nyingine mbalimbali za Afrika.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu mkuu wa BFT, Makore Mshaga amesema, baada ya kumaliza mapambano ya kirafiki, wataandaa mashindano maalum yatakayoyashirikisha mataifa zaidi ya matano kwa nia ya kuwapa mabondia wa Tanzania uzoefu wa kuweza kushiriki mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Congo Brazzaville Septemba nne mpaka 19 mwaka huu.

Mashaga amesema ili kuweza kuwajenga zaidi vijana hao, wamepata mualiko nchini Serbia katika mashindano ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika Julai mwaka huu ambapo itakuwa na tija kubwa kwa mabondia hao ambao anaamini wataweza kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika.

Mashaga amesema, kwa upande wa timu ya wanawake ambao wanatarajia kushiriki mashindano ya Olimpiki yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2016 nchini Brazili wamewaandalia programu maalumu ambapo wataanza na mashindano ya Taifa yatakayofanyika Mei 17 mpaka 24 mwaka huu.