
Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, mchakato huo utasimamiwa na kamati ya uchaguzi ya Yanga chini ya uangalizi wa kamati ya uchaguzi ya TFF huku wale waliochukua fomu za kuwania uchaguzi kupitia TFF Wakitakiwa kushirikishwa katika uchaguzi huo.
Lucas amesema, katika mchakato huo Yanga inatakiwa kutumia katiba ya mwaka 2010 katika uchaguzi huo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Rais wa TFF Jamal Malinzi, Katibu wa TFF Mwesigwa Celestine, Kaimu mkurugenzi wa masuala ya sheria na uanachama Eliud Mvela huku kwa upande wa Yanga alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga na Katibu wa Yanga Baraka Deusdedit.
Mvutano uliibuka kuhusu uchaguzi wa Yanga SC kiasi cha kuwaacha njia panda wanachama wa klabu hiyo, wakiwa hawajui washike lipi, baada ya TFF kutangaza na kuendesha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo wakati huo huo klabu hiyo nayo ikitangaza na kuendesha mchakato wake huo yenyewe.
Yanga ilisema uchaguzi wake utafanyika Juni 11 na TFF ikasema utafanyika Juni 25 huku wote wakianza kugawa fomu za kugombea wiki iliyopita.
Waliochukua fomu TFF ni Aaron Nyanda, Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wakati miongoni mwa waliochukua fomu Yanga ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayoub Nyenzi.