Tuesday , 8th Dec , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania mchezo wa tenisi kwa walemavu inatarajiwa kuondoka nchini Desemba 13 mwaka huu kuelekea nchini Afrika Kusini kwenye mashindano ya BMP Parabous ikiwa ni ya kusaka pointi ili kujiimarisha kwenye viwango vya ubora wa dunia.

Timu ya taifa ya walemavu ikiagwa ikielekea mashindano ya All African Games iliyofanyika mwaka huu nchini Congo Brazzaville

Akizungumza na East Africa Radio kocha mkuu wa kikosi hicho Riziki Salum amesema mchakato unaendelea vyema licha ya uwezeshwaji kuwa mdogo hali inayopelekea kuondoka na wachezaji saba badala ya 12 aliopanga awali.

Aidha kocha huyo ameomba wadau kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwanunulia vifaa ambavyo vitawawezesha wao kushiriki vyena na kupata ponti nyingi zitakaiwezesha Tanzania kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Olimpiki ya Rio mwakani.

Timu ya Tanzania ya walemavu inayojumuisha wachezaji wa kiume na wa kike itakuwa nchini Afrika Kusini kwa siku sita kwenye mashindano hayo muhimu kwa taifa ambayo yanajumuisha mataifa yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 kwenye mchezo huo wa tenisi.