Thursday , 16th Jun , 2016

Baada ya kutembeza bakuli kuomba udhamini wa safari ya kwenda kushiriki michuano ya wazi ya Kenya timu ya taifa ya tenisi kwa walemavu ya Tanzania imeondoka leo alfajiri kuelekea Nairobi nchini Kenya baada ya kudhaminiwa.

wachezaji wa tenisi kwa walemavu wakicheza.

Wachezaji 11 na kocha mmoja wa timu ya mchezo wa tenisi kwa upande wa walemavu ya Tanzania wameondoka kuelekea nchi Kenya kushiriki michuano ya kimataifa ya wazi ya Kenya Open itakayoanza Juni 18 mwaka huu.

Wakizungumzia michuano hiyo kocha mkuu wa kikosi hicho Riziki Salum amesema pamoja na wachezaji wake kupitia changamoto nyingi wakati wa maandaizi yao kuanzia mazoezi na hadi kuelekea safari hiyo ni kwamba vijana wote wako tayari kwa mashindano hayo makubwa na wanataraji kuendelea kuwika kama kawaida yao.

Riziki amesema kikosi hicho kitakuwa na wachezaji 6 wa kiume na 5 wakike na wanakwenda huko kama mabingwa watetezi na vinara wa mchezo huo kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kati kwa upande wa walemavu.

Naye nahodha wa timu hiyo Vosta Peter akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake ameomba Watanzania wote kwa ujumla wao wawaombee dua na wao watatimiza kile ambacho kimewapeleka nchini humo ikiwemo kutwaa ubingwa huo na kuendelea na rekodi ya kuwa vinara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Wakimalizia Kocha Riziki Salum na nahodha wake Vosta Peter wamewashukuru wadau wote kwa kuwawezesha kwa namna moja ama nyingine kuweza kwenda katika mashindano hayo makubwa na wameahidi kulipa fadhila na pia wametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuisaidia timu hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi hasa vifaa.