Thursday , 30th Apr , 2015

Timu ya taifa ya kuogelea ya Tanzania inatarajia kushiriki michuano ya Kanda ya 4 itakayofanyika Luanda, Angola kuanzia Mei 6 hadi 9 mwaka huu.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu mkuu wa chama cha kuogelea nchini TSA, Noel Kiunsi amesema, Michuano hiyo itakuwa ni sehemu ya kufuzu kucheza michezo ya Afrika itakayofanyika nchini Congo Brazzaville mwezi Septemba.

Kiunsi amesema wachezaji waliochaguliwa na TSA kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ni Sylivia Raphael, Smriti Gokarn, Collins Saliboko na Josephine Oosterhuis ambapo kwa sasa wanafanya mazoezi ili kujiandaa vema na ushindani kutoka nchi nyingine ikiwemo Uganda.

Kiunsi amesema, wana imani wachezaji hao watafanya vizuri ambapo mchezo wa kuogelea umekuwa ni miongoni mwa michezo inayokuja juu nchini Tanzania huku wachezaji wake wakishiriki michuano mbalimbali kama vile ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Glasgow na michezo ya Olimpiki iliyofanyika London, Uingereza.