Saturday , 4th Jun , 2016

Kweli la kuvunda halina ubani. Hi ni baada ya ndoto za timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kushiriki michuano ya kimataifa kufutika rasmi kufuatia kupoteza mchezo muhimu kabisa dhidi ya Misri uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mfungaji wa magoli yote ya Misri Mohamed Salah.

Timu ya taifa ya Misri imekata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon, baada ya kuwafunga wenyeji, Tanzania mabao 2-0 jioni ya leo uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na pointi 10 baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoa sare moja, wakati Tanzania inabaki na pointi yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria yenye pointi mbili.

Hadi mapumziko, Misri walikuwa wanaongoza kwa bao lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea ya Uingereza ambaye kwa sasa anachezea timu ya AS Roma ya Italia, Mohammed Salah kunako dakika ya 43 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki Mwinyi Hajji Mngwali kumkwatua nje kidogo ya boksi mchezaji Nagram Fahmy.

Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kila upande ulipoteza nafasi za wazi.

Dakika ya 27, mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu aliunganishia juu ya lango krosi ya Elias Maguri na dakika ya 30, nahodha Mbwana Ally Samatta alipewa pasi nzuri na Farid Mussa akapiga nje.

Taifa Stars ilianza kipindi cha pili vizuri na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 53 iliyotolewa baada ya kiungo Himid Mao kuangushwa na Ame Medhat hata hivyo, mkwaju wa nahodha Samatta ulipanguliwa na kipa mkongwe barani, Essam Kamal Tawfik.

Salah alifunga bao la pili la Misri mnamo dakika ya 58 baada ya kumpita beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyecheza chini ya kiwango siku ya leo.

Tanzania katika mchezo wa hii leo; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk68, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.

Misri; Essam Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel, Mohamed Abdel Sayed, Abood Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed Ibrahim, Abdallah Mahamoud Said na Nagram Mohsin Fahmy.