Thursday , 2nd Jul , 2015

Kikosi cha wachezaji 20 cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimeondoka nchini jioni ya leo kuelekea Kampala nchini Uganda kwa ajili ya mchezo wake wa marudiano dhidi ya The Cranes siku ya jumamosi.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha wa Stars, Charles Mkwasa amesema, Kikosi cha Taifa Stars kinaondoka na idadi hiyo ya wachezaji pamoja na bechi la ufundi la watu saba huku akiwaacha baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi.

Mkwasa amesema, vijana wake wamefanya mazoezi vizuri katika kipindi chote cha maandalizi, na sasa wako tayari kwa mchezo huo, mipango ikiwa ni kupata ushindi siku ya jumamosi katika mechi hiyo ya marudiano kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Rwanda.

Mkwasa amesema, katika msafara huo atawakosa wachezaji wawili, Abdi Banda na Mohamed Hussein (Tshabalala) waliopata majeruhi wakati wa mazoezi huku nafasi zao zitazibwa na wachezaji waliopo kambini.

Kwa upande wake, Nahodha wa Stars, Nadir Haroub Canavaro amesema, wanajua wanasafari kubwa kutokana na matokeo ya awali kwani mechi na Uganda ni mechi ngumu lakini watajitahidi kupata matokeo mazuri ili kurejesha imani kwa watanzania pamoja na kuwa katika nafasi nzuri.

Wachezaji wanaosafiri ni: Ally Mustafa, Mudathir Khamis, Juma Abdul, Shomari Kapombe, Haji Mngwali, Michael Aidani, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Frank Domayo, Mudathir Yahya, Salum Telela, Said Ndemla, Saimon Msuva, Deus Kaseke, Ramadhan Singano, Atupele Green, Rashid Mandawa, John Bocco na Ame Ally.