Monday , 11th Jun , 2018

Katika kukuza na kuendeleza mpira wa Kikapu nchini kampuni ya East Africa Television LTD, kwa kushirikiana na kinywaji cha Sprite leo Jumatatu Juni 11, imezindua msimu wa pili wa mashindano ya Sprite Bball Kings 2018.

Akizungumza katika uzinduzi huo Meneja masoko wa EATV Basilisa Biseko amesema,  lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji na kuutangaza mchezo huo nchini ambapo mshindi wa kwanza atajishindia zawadi ya shilingi Millioni kumi.

“Ninayo furaha kuzindua msimu wa pili wa mashindano ya Sprite Bball Kings 2018 ambapo kwa mwaka huu usaili wa timu shiriki, utafanyika kwa siku moja ya Jumamosi Juni 16, katika viwanja vya Mlimani City Mall kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni”, amesema Basilisa.

Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya Cocacola ambao ndio wadhamini kupitia kinywaji chake cha Sprite Sialouise Shayo amesema kuwa watahakikisha wanaongeza jitihada zaidi katika kukuza mchezo huo na kufanikisha kuzunguka nchi nzima hapo baadaye.

Naye Katibu Mkuu kutoka shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) Michael Mwita amesema, matunda ya Sprite Bball Kings yameonekana hivyo yanatakiwa kuungwa mkono na kuthaminiwa katika sekta ya michezo.

“Nimepata jumbe nyingi sana kutoka kwa vijana na wapenzi wa mpira wa Kikapu wakiulizia michuano hii lakini leo naamini watafurahi kusikia taarifa hizi na watajitokeza kwa wingi siku ya usaili”, amesema Mwita.