Friday , 1st Dec , 2017

Klabu ya soka ya Simba inatarajia kumtangaza mshindi wa zabuni ya kuwekeza kwenye klabu kupitia mkutano mkuu wa klabu, utakaofanyika jumapili Desemba 3, 2017.

Akiongea na waandishi wa habari leo msemaji wa klabu hiyo Haji Manara, amesema mchakato wa kumtafuta mwekezaji umekamilika na jumapili klabu itamtangaza na wataingia kwenye mfumo mpya wa uendeshaji.

“Tutafanya mkutano mkuu siku ya jumapili, mkutano ambao una agenda moja tu ya kumtangaza mshindi wa zabuni ya kuwekeza kwenye klabu, mchakato huu umepitia mambo mengi lakini jumapili tutamtangaza”, amesema Manara.

Manara amesema tayari wameshapata ruhusa ya kuendelea na mchakato huo kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na waziri Dkt. Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo.

Mkutano huo mkuu wa klabu utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam ambapo rasmi klabu hiyo itahamia kwenye mfumo mpya wa kuendesha klabu kwa hisa.