Mechi ya mzunguko wa kwanza kati ya Simba na Mbao
Katika mchezo huo Simba SC ilionekana kuelemewa katika kipindi cha kwanza cha mchezo na kusababisha wapinzani wao kujipatia bao la kwanza likifungwa na George Sangija katika dakika ya 18 ya mchezo na ilipofikia dakika ya 33 waliweza kupachika bao la pili kupitia Evarigestus Bernald na kufanya kuongoza kipindi chote cha kwanza.
Katika kipindi chote cha kwanza, Simba walionekana kutokuwa na utulivu na kucheza kandanda lisiloeleweka, hali ambayo huenda ilichangiwa na kikosi kilichoanza leo kuwa tofauti kuanzia golini ambapo alikaa Manyika Peter, huku ulinzi wa kati ukifanywa na Besala Bukungu na Mlinzi wa kulia akiwa Amadi Juma.
Pia katika safu ya ushambuliaji, leo mwalimu wa Simba aliwaanzisha Juma Luizio na Pastory Athanas ambao walionekana kutokuwa fiti kimchezo, na kulazimika kufanya mabadiliko ya mapema, ambapo waliingia Fredrick Blagnon, Laudit Mavugo na Said Ndemla
Ikiwa na mabadiliko hayo baada ya kurudi kipindi cha pili Simba SC ilionesha jitihada zake za makusudi kuchungulia goli la wapinzani wake na kuzaa matunda katika dakika 82 ya mchezo kupitia mshambuliaji wake Fredrick Blagnon.
Kutokana na matukio ya kuanguka mara kwa mara kwa wachezaji wa Mbao, mwamuzi aliamua kuongeza dakika 7 baada ya 90 kumalizika ambapo katika dakika hizo 7 za nyongeza Simba SC ilionekana kupata uhai zaidi na nguvu huku ikicheza 'jihadi' na hatimaye kupata mabao mawili dakika ya 3 ya nyongeza kupitia kwa Blagnon tena.

Fredrick Blagnon
Ilipofikia dakika 90 (+6) Simba waliweza kuwainua tena mashabiki zao kupitia Mzamiru na kufanya uwanja wote kutimuka vumbi kwa kushangalia ushindi huo wa kihistoria.
Kutokana na matokeo hayo Simba imefikisha alama 58 na kuifanya kuwa kileleni huku Yanga FC wakirudi nafasi ya pili kwa alama zao 56 wakiwa na mchezo mmoja mkononi huku Kagera Sugar wakibakia nafasi yake ile ile ya tatu kwa alama 45 Baada ya Azam FC kulazimishwa suluhu na Mtibwa katika mchezo uliopigwa leo Manungu, Morogoro.








