Sunday , 21st Oct , 2018

Klabu ya Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya 'Wapiga debe' Stand United katika uwanja wa taifa katika muendelezo wa ligi kuu Tanzania bara.

Wachezaji wa Simba wakifurahia ushindi

Mabao ya Simba katika mchezo huo yamefungwa na kiungo, Clatous Chama katika dakika ya 30, Emmanuel Okwi katika dakika ya 45 na bao la tatu likisababishwa na mchezaji wa Stand United, Erick Mulilo aliyejifunga  katika dakika ya 78.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa kuvutia kutokana na timu zote kucheza kwa staili moja ya kushambulia huku Simba ikionekana kutawala zaidi kwa mashambulizi hasa katika kipindi cha pili.

Kwa matokeo hayo, Simba inafikisha alama 17 na kukwea hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi. Azam Fc inaongoza ligi kwa alama zake 21 ikifuatiwa na Yanga yenye alama 19.

Ratiba ya michezo mingine ni, Mbao Fc ambayo imeibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar huku mchezo wa mapema kabisa ukishuhudiwa Lipuli Fc ikifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika uwanja wake wa nyumbani wa Samora.