Sunday , 25th Mar , 2018

Vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara, klabu ya Simba baada ya mapumziko ya siku sita imeanza mazoezi huku ikiwa inawakosa nyota wake kadhaa ambao wapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa.

Kikosi hicho cha Simba kimeanza rasmi mazoezi hayo ya kujiandaa na mwendelezo wa ligi kuu jana jioni, kwenye uwanja wa Boko jijiini Dar es Salaam kikiwa na nyota ambao hawajaitwa kwenye timu zao za taifa.

Baadhi ya wachezaji ambao Simba inawakosa ni mshambuliaji Emmanuel Okwi na mlinzi Juuko Murshid ambao wapo na timu ya taifa ya Uganda ambayo jana ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sao Tome and Principe na kushinda mabao 3-1.

Wengine ni nyota wa Taifa Stars ambao wanajiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo, Said Ndemla, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya na Erasto Nyoni.

Simba ambayo inaongoza ligi ikiwa na alama 46 inatarajia kushuka kwenye dimba la Sabasaba mjini Njombe kucheza na wenyeji Njombe Mji kwenye mchezo wa ligi kuu April 3 mwaka huu.