Wednesday , 3rd Feb , 2016

Serikali imetakiwa kuweka kipaumbele katika mchezo wa Tenisi ili kuweza kupata vijana wengi watakaoweza kufanya vizuri katika mchezo wa Tenisi kama ilivyo michezo mingine hapa nchini.

Kocha wa tenisi kwa timu za vijana Hassan Kassim amesema, wizara ya michezo ya nchi inatakiwa kusaidia vijana walio ndani ya mchezo huo badala ya kuwaachia viongozi wa vyama ambao wakimaliza muda wao wanaondoka na vipaji vya vijana vinashuka kwa kukosa wawekezaji.

Kocha Kassim amesema, vyama vya mikoani vimekuwa vikisaidiwa na viongozi suala linalochangia kuendelea kupoteza vijana katika mchezo huo hususani kwa upande wa mikoani kwani mikoani viongozi sio wengi kama ilivyo kwa Dar es salaam ambapo viongozi hushirikiana na wazazi kwa karibu kwa ajili ya kusaidia vijana hao.

Kocha Kassim amesema, iwapo serikali itazingatia katika kusaidia mchezo huo, nchi itaweza kupata vijana wengi na wazuri watakaoweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali makubwa ya ndani na nje ya nchi na kuweza kushindana kimataifa.