Wachezaji wa Savio.
Timu ya Savio imeibuka mshindi wa tatu katika ligi ya klabu bingwa ya taifa ya kikapu NBL baada ya kuifunga timu ya Bandari kutoka Tanga kwa vikapu 59-49, michuano iliyopigwa katika uwanja wa ndani wa taifa jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Mchezo huo,Nahodha wa timu ya Savio Roma Anania amesema lengo lilikuwa kuingia fainali ya michuano hiyo lakini wameambulia mshindi wa tatu licha ya kuwa na majeruhi katika timu yake hali ilichangia wapinzania wao kuongoza kwa vikapu vingi katika robo ya kwanza na ya pili ya mchezo huo.
Naye Nahodha wa timu ya Bandari Alphonce Kusekwa amesema michuano ya mwaka huu imekuwa na msisimko mkubwa kutokana na timu nyingi kutoka mikoani kushiriki katika michuano hiyo ikiwa ni pamoja na timu yao huku wakiwa wamejipanga kushindana na si kushiriki hali ilichangia kuonyesha ushindani wa kutosha kwa timu za Dar es salaam.
Mchezo huo ulitanguliwa na Mchezo wa Mshindi wa tatu kwa wanawake,ambapo timu ya Vijana Queens wameibuka washindi baada ya kuibugiza timu ya Tanga Queens kwa vikapu 97-58 huku Nahodha wa Tanga Queens Blandina Seme akisema uzoefu ndio uliowaangusha katika mchezo wa leo.