Akizungumzas na East Africa Radio, Mkurugenzi wa michezo wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Boniface Wambura amesema timu zitapumzika kwa siku ya kesho ambapo Jumatano zitacheza hatua ya Robo fainali huku Fainali ikitarajiwa kuchezwa Ijumaa ya wiki hii katika Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Wambura amesema lengo hasa la michuano hiyo sio kutafuta mshindi pekee kwa vijana hao ila lengo kubwa hasa ni kutoa fursa kwa wachezaji vijana kuonesha uwezo wao wa kucheza mpira na kuonesha vipaji ili wengine waweze kuviona na kuviendeleza.
Wambura amesema michuano hiyo imetawaliwa na kanuni zinazotakiwa kufuatwa ili kuweza kuboresha michuano hiyo, ikiwemo suala la umri ambapo kuna mikoa miwili ya Mbeya na Lindi, imeondolewa katika michuano hiyo kutokana na kushindwa kuthibitisha kama ni kweli wana umri chini ya miaka 15 au wamezidi.
Wambura amesema kanuni za mashindano zinahitaji kila timu iwe na wachezaji 16 hivyo kama wachezaji wana kasoro na timu ikawa na wachezaji pungufu, timu hiyo haitaruhusiwa kushiriki mashindano hayo.