Kikosi cha timu ya taifa ya riadha kimeanza kujikusanya kambini kwenye chuo cha misitu mkoani Kilimanjaro.kwa ajili ya kujiandaa na michuanio ya Olympic mjini Rio baadaye mwaka huu.
Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha riadha Tanzania RT, Bi Ombeni Zavara, amesema kambi hiyo imeanza Februari 10 mwaka huu na itaenda hadi mwezi Agost mwaka huu, kabla ya kuelekea Brazil mwezi huo.
Zavara amesema katika kambi hiyo kutakuwa na wachezaji 14, watatu ni wanawake,na tayari wengine wameshawasili
Akiwataja baadhi ya wachezaji waliofika kambini kuwa ni Fabian Joseph, Alphonce Felix, Saidi Juma na wachezaji wawili wakiongezwa ambao ni Ali Ghulam mita 100 kutoka Zanzibar na Angelina Sele mshindi wa mbio za 'Hapa Kazi Tu' na wengine wakitarajiwa kuwasili.
Hadi sasa kambi hiyo ina wachezaji wawili pekee wenye sifa za kucheza Olympic ambao ni Alphonce Felix na Juma Said.
Zavara amesema ili kupata wachezaji wengine wa kuungana na waliofuzu, kutakuwa na mashindano baadaye mwezi huu kwa ajili ya kutafuta vigezo na kwamba hadi kufikia Mei 30 mwaka huu inatakiwa kuwe kumeshapatikana wachezaji wenye sifa za kucheza Olympic mjini Rio.





