Saturday , 27th Dec , 2014

Timu ya Polisi Morogoro inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara imepania kuibuka na ushindi katika mchezo wake wa kesho dhidi ya mgambo JKT kwa kuonesha kandanda la kuvutia.

Msemaji wa timu ya Polisi Morogoro, Mwanaidi Lwena

Baada ya kupata mchanganyiko wa askari na raia katika safu yake ya uongozi, timu ya soka ya Polisi Morogoro imekusudia kufanya maajabu kwenye mchezo wa ligi kuu soka ya vodacom kati yake na Mgambo JKT, utakaopigwa Jumapili, kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Msemaji wa timu ya Polisi Morogoro, Mwanaidi Lwena, amesema timu hiyo inafungua awamu ya pili ya pazia la ligi kuu, ikiwa na ari mpya, baada ya kumaliza uchaguzi wake uliohusisha raia na askari, ikiwa ni baada ya kupata wanachama wapya, ambapo ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani hapo, kushuhudia kandanda safi itakayooneshwa na kikosi cha Polisi Morogoro katika mchezo wake na maafande wa Mgambo.

Katika hatua nyingine timu za mchezo wa kikapu mkoani Morogoro, zimeanzisha bonanza maalum kwaajili ya kusaka vipaji vya kuwaibua wachezaji wapya wa mchezo huo, na kubainisha pamoja na mikakati hiyo, pomoja na faida zilizopo, bado zipo changamoto ambazo zinawakabili waibuaji hao wa vipaji, ikiwemo mwamko mdogo wa wachezaji wa kike na maeneo ya kufanyia mazoezi hususani viwanja vyenye sifa kukidhi mchezo huo..