Wednesday , 10th Oct , 2018

Kocha mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema anasikitika kwa kitendo cha mashabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani kushangilia matokeo baada ya mchezo lakini anafurahi kwasababu hawakuja kufanya vurugu.

Mashabiki wa Coastal Union.

Hivi karibuni shirikisho la soka nchini Tanzania TFF liliipa onyo klabu hiyo kutokana na kitendo cha mashabiki wake kuingia uwanjani kushangilia matokeo baada ya mchezo kumalizika, kitendo ambacho ni kinyume na kanuni za mashindano za shirikisho hilo.

Akizungumza na www.eatv.tv kuhusiana na namna anavyoichukulia adhabu hiyo, kocha huyo amesema,

"Kinachonisikitisha ni kwamba tumevunja kanuni lakini kikubwa ambacho wanacho mashabiki wetu ni ule mhemko, wana mihemko mikubwa ya kuipenda timu yao. Hata shitaka lenyewe utaliona, ni kwamba wameshitakiwa kwa kosa la kuingia uwanjani na si kufanya fujo".

"Lakini kubwa na ninachofurahi ni kwamba hata shitaka lenyewe linasema kwamba wapenzi wa Coastal Union waliingia uwanjani kwenda kuwapongeza wachezaji wao na sio kufanya fujo tofauti na watu wengine mnavyotafsiri". Ameongeza kocha huyo.

Kocha huyo pia amekisifia kikosi chake kuwa kinakwenda mwenendo mzuri katika ligi kutokana na vijana wake kuwa na umri mdogo unaowapa nguvu na molari ya kufanya vizuri. Coatal Union itamenyana na JKT Tanzania, mchezo utakaopingwa 20, Oktoba.