Mabondia Karama Nyilawila kushoto na Said Mbelwa kulia wakiwa na mwamuzi wa pambano lao la UBO Anthony Rutha.
Kampuni inayosimamia ngumi za kulipwa nchini PST iliyosimamia pambano la ubingwa wa kimataifa wa UBO lililovunjika baina ya bondia Karama Nyilawila wa Dar es salaam na Said Mbelwa wa Tanga hii leo imemkabidhi rasmi mkanda huo bondia Karama Nyilawila
Rais wa PST Emmanuel Mlundwa kabla ya kukabidhi mkanda huo amesema pamoja na kumpa ushindi Nyilawila lakini walilazimika kutoa adhabu mbili kwa bondia Mbelwa kutokana na kuvunja sheria za mchezo wa ngumi za kulipwa
Mlundwa amesema kwanza wamemtaka bondia Mbelwa kurejesha fedha aliyolipwa na promota kwa ajili ya pambano hilo kupitia PST ambao watazirejesha kwa promota huyo na pili PST imemsimamisha bondia huyo kufanya kazi na kampuni hiyo kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia may 25 hadi novemba 25 mwaka huu.
Naye bondia Karama Nyilawila mara baada ya kukabidhiwa mkanda huo pamoja na kuwashukuru PST kwa kusimamia haki na kwa kufuata sheria za ngumi za kulipwa amejinasibu kuwa yuko tayari kuendelea kutwaa mikanda mikubwa ya kimataifa na hivyo amewaomba mapromota kumtafutia mapambano ya kimataifa kwa kumpambanisha na mabondia bora
Pambano hilo lilichezeshwa na mwamuzi mzoefu Anthony Rutha ambaye amethibitisha ukweli juu ya kilichotokea na amesema kamwe hakuchezesha pambano hilo kwa kumpendelea mtu yeyote na alizingatia sheria zote za ngumi za kulipwa.