Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Aishi Manula
Timu ya soka ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes leo (Jumapili May 11, 2014) imepoteza mchezo wake dhidi ya vijana wa Nigeria Flyng Eagle baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0.
Mechi hii ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 imepigwa leo Jumapili (Mei 11 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kushuhudia Vijana hao wa Tanzania wakishindwa kabisa kutamba katika dimba la nyumbani.
Magoli yote ya Nigeria hii leo yamepatikana katika kipindi cha pili, ambapo Yahya Mussa amefungua kitabu hicho cha mabao kunako dakika ya 48 ikiwa ni dakika tatu tangu kuanza kwa kipindi cha pili baada ya uzembe kufanyika katika safu ya ulinzi ya Ngorongoro Heroes.
Bao la pili kwa Nigeria limefungwa na Mohamed Mussa dakika ya 82 baada ya kutumia vyema makosa ya Pascal Ngonyani wa Ngorongoro Heroes na kuipa mtihani mzito wa kujiandaa katika mechi ya marudiano.
Licha ya kupoteza mchezo huo, vijana wa Ngorongoro Heroes walionesha Kandanda safi japo halikuwa na malengo ya kutumia nafasi walizopata kutengeneza magoli.
Safu ya ushambuliaji ya Ngorongoro Heroes iliyoongozwa na Kelvin Friday ilipoteza nafasi kadhaa za kufunga kutokana na kutokuwa na umakini wa kutosha.
Katika mchezo huu Ngorongoro Heroes ilipata pigo baada ya nahodha wake na golikipa namba moja Aishi Manula kuumia hali iliyolazimu benchi la ufundi kumtoa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Manyika Peter.
Kwa matokeo haya Ngorongoro Heroes imejiweka katika nafasi finyu ya kufuzu mashindano ya Afrika kwa vijana yatakayofanyika mwakani nchini Senegali, kwani inahitaji kushinda zaidi ya magoli matatu kwa bila ili iweze kusonga mbele.
Fainali hizo za 19 za Afrika zitafanyika mwakani nchini Senegal zikishirikisha timu saba zitakazofuzu kwenye mechi za mchujo, na Senegal wanaoingia moja kwa moja kutokana na kuwa wenyeji.