Monday , 21st May , 2018

Nyota wa kimataifa wa Tanzania Simon Msuva usiku wa jana, amecheza mchezo wa mwisho kwenye ligi kuu ya soka nchini Morocco na kuifungia bao timu yake ya Difaa Hassan El Jadida dhidi ya Olympic Safi.

Msuva alifunga bao hilo dakika ya 43 katika mchezo huo wa ligi hiyo maarufu kama Botola Pro uliofanyika Uwanja wa Ben Ahmed El Abdi, El Jadida mjini Mazghan.

Pamoja na ushindi huo wa bao 1-0 lakini haujaisadia timu hiyo kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, baada ya kumaliza katika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa ligi ya nchini humo.

Difaa Hassan El Jadida imefikisha pointi 48 baada ya kucheza mechi 30 na ipo nyuma ya FUS Rabat yenye pointi  49, Hassania Agadir pointi 51 sawa na Wydad Casablanca.

Difaa msimu huu inashiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Africa na ilitoka sare ya 1-1 na MC Alger nchini Algeria na kufungwa 2-0 nyumbani na TP Mazembe. Timu hiyo itakamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza wa kundi  B kwa kumenyana na ES Setif nchini Algeria Julai 17.