Friday , 19th Oct , 2018

Rais Magufuli amekabidhi fedha hizo leo, Oktoba 19, 2018 Ikulu jijini Dar es salaam alipowaalika wachezaji wa timu hiyo huku akiweka wazi kuwa wameingia kwenye mkataba mgumu na wasiposhinda watazitapika fedha hizo.

Wachezaji wa Taifa Stars kushoto na Rais Magufuli kulia.

''Nawakabidhi shilingi milioni 50, nahodha wa Taifa Stars na Rais wa TFF mbele ya Waziri Mwakyembe hapa hapa muondoke nazo lakini mkashinde na zitumike vizuri kwaajili ya wachezaji, msiposhinda niwaambie kabisa mtazitapika kwa namna nyingine'', amesema Rais.

Aidha katika hafla hiyo Rais amewataka wachezaji kujituma zaidi huku akiwaeleza wazi kuwa hajafurahishwa na matokeo ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde hapa nyumbani kwani bado tunadaiwa bao 1 baada ya kufungwa mabao 3-0 ugenini.

Pia Rais amewataka Rais wa TFF, Wallace Karia na Waziri mwenye dhamana ya michezo Harrison Mwakyembe kuhakikisha timu hiyo inafuzu AFCON 2019 kwa kushinda mechi mbili zilizobaki dhidi ya Uganda na Lesotho.

Taifa Stars ambayo ipo kundi L na timu za Uganda, Cape Verde na Lesotho, ina alama 5 katika nafasi ya pili nyuma ya Uganda yenye alama 10 kileleni.