Friday , 13th Nov , 2015

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania Charles Boniface Mkwasa amesema, yote waliyokuwa wakiyafanya walipokuwa kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya Algeria watayafanyia kazi hapo kesho ili kuweza kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Mkwasa amesema, anaamini mchezo utakuwa ni mgumu lakini kwa mazoezi na juhudi kwa wachezaji wanaamini wataibuka na ushindi.

Kwa upande wake mshambuliaji Mbwana Samatta amesema, mechi ya kesho itakuwa nzuri kutokana na wachezaji kujiandaa ambapo ameongeza kuwa na mechi mfululizo bila kupata muda wa kupumzika haiathiri mchezo wa kesho au wa marudiano kwani wameshazoea na ni kazi yao.

Kwa upande wake Mlinda Mlango Aishi Salum Manula amesema, kambi ya Afrika Kusini imewasaidia na kila mchezaji yupo vizuri kilichobakia ni kwa kila mchezaji kujitambua kuwa anawakilisha taifa na anatakiwa kufanya vizuri katika mchezo huo ili kuwafunga Algeria nyumbani na hata katika mchezo wa marudiano Novemba 17 nchini Algeria.