Saturday , 25th Oct , 2014

Mashindano ya wazi ya taifa ya kuogelea yameanza hii leo jijini Dar es salaam huku yakishirikisha vilabu 13 na waogeleaji binafsi zaidi ya 53 toka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Waogeleaji wakichuana katika michuano ya kuogelea jijini Dar es salaam.

Mashindano hayo yamekuwa na msisimko mkubwa baada ya washiriki katika makundi yote kuonesha uwezo wa hali ya juu na ushindani wa aina yake

Katibu mkuu wa chama cha kuogelea Tanzania TSA Noel Kihunsi amesema mashindano hayo yamegawanywa katika makundi kulingana na umri kuanzia miaka 6 hadi watu wazima huku wakitazama zaidi kukuza vijana wadogo kwani ndio lengo la mashindano hayo kwa mwaka huu ikiwa ni mikakati ya TSA kupata vipaji vipya watakavyoviendeleza kwaajili ya timu za taifa katika michuano ijayo.

Naye Jerry Junior mmoja wa wachezaji ambao wamefanya vema katika mchuano huo amesema ushindani ni mkubwa sana katika michuano ya msimu huu kitu ambacho kitasaidia kuinua mchezo huo hasa kwa vijana na hali hiyo amesema imechangiwa na wachezaji kufanya maandalizi yakutosha.

Naye mmoja wa wazazi ambao walikuwa mashuhuda wa michuano huyo Bi Roselyne Muriya amesema michezo kwa vijana ni fursa kwao kupata mazoezi ya kutunza afya zao na pia sasa michezo ni ajira hivyo anatoa wito kwa wazazi wote kuwaacha watoto wacheze na kutumia fursa ya vipaji walivyonavyo kuwabadilishia maisha.