Michael Wambura akiwa na baadhi ya wanachama wenzake waliofutwa uanachama na mkutano mkuu wa klabu ya Simba.
Zikiwa zimepita siku mbili tangu mkutano wa wanachama wa klabu ya soka ya Simba kuwafuta uanachama wanachama 71 wa klabu hiyo akiwemo Michael Richard Wambura hii leo Michael Wambura ameibuka na kusema hatambui maamuzi hayo kwani ni maamuzi ya kupangwa na kikundi cha watu fulani wasioitakia mema klabu ya Simba kwa maslahi yao binafsi
Akiongea jijini Dar es salaam Wambura amesema maamuzi hayo ni batili kwa sababu mkutano huo haukufafanua ni katiba gani imetumika kutoa maamuzi hayo kwakuwa wanachama hao akiwemo yeye walikwenda mahakamani kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2010 na 2014
Aidha Wambura amesema kimsingi uongozi wa klabu ya soka ya Simba unahitaji kutumia busara ya hali ya juu kama kweli wanataka kuinusuru klabu hiyo isitumbukie katika mgogoro mzito kwani kuwafuta uanachama sio suluhisho kwakuwa tatizo lililowafanya wanachama hao kwenda mahakamani bado litakuwepo
Wambura amesema kwa sasa anasubiri taarifa za uongozi wa Simba kuhusu maamuzi ya mkutano uliowasimamisha ili ajue cha kufanya na ameshawasiliana na wanasheria wake ili apate ushauri wa nini cha kufanya kwa mujibu wa sheria na baadaye wakati wowote atatoa tamko la mwisho ama uamuzi wake juu ya jambo hilo.