Kocha mpya wa Taifa Stars, Mart Nooij
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza rasmi Mart Nooij kutoka Uholanzi kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais wa TFF, Jamal Malinzi amemtambulisha kocha huyo leo (Aprili 26 mwaka huu) kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akiwa amefuatana na Makamu wake Wallace Karia, amesema anafurahi kumtangaza Nooij na ana matarajio kuwa Tanzania itanufaika na uzoefu wake mkubwa wa ukocha, hasa katika bara la Afrika.
“Nawaahidi Watanzania kuwa sitomuingilia kocha katika kazi yake. Kama mimi sitomuingilia kocha, basi hakuna mtu yeyote atakayemuingilia. Tumemwajiri yeye kwa vile ni mtaalamu, hivyo hakuna sababu ya kumuingilia,” amesema Rais Malinzi.
Naye Nooij ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili amesema yeye ni mtu wa maneno mafupi, hawezi kuahidi kitu lakini ana matarajio ya kuifanya Taifa Stars ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali.
Amesema kabla ya kukubalia kufundisha Taifa Stars alikuwa na klabu ya St. Georges ya Ethiopia, lakini vilevile amewahi kufundisha mpira wa miguu barani Afrika katika nchi za Burkina Faso, Mali na Msumbiji.