Sunday , 21st Oct , 2018

Imethibitika kuwa nyota wa Barcelona, Lionel Messi atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu baada ya kuumia jana katika mchezo wa La Liga dhidi ya Sevilla.

Lionel Messi na Cristiano Ronaldo

Messi amepata jeraha la mkono wa kulia baada ya kuanguka kwa nguvu kwenye mchezo huo ambao Barcelona ilishinda kwa mabao 4-2 katika uwanja wa Camp Nou.

Kutokana na jeraha hilo, Messi ataukosa mchezo wa klabu bingwa Ulaya Jumanne ijayo dhidi ya Inter Milan pamoja na mchezo wa  El Clasico wikiendi ijayo na michezo mingine itakayofuatia.

Huku upande wa Real Madrid ukimkosa nyota wake Cristiano Ronaldo ambaye amejiunga na Juventus msimu huu. Kwa pamoja, nyota hao wanaweka historia mpya kwenye mchezo wa El Clasico, ambapo ni kwa mara ya kwanza kwa mchezo huo kuchezwa bila ya uwepo wa nyota hao wawili au mmoja wapo tangu mwaka 2007.

Pia Barcelona haijawahi kushinda mchezo wowote wa El Clasico bila ya uwepo wa Messi, tangu mchezaji huyo alipoanza kuichezea klabu hiyo mwaka 2004.

Timu hizo zitakutana wikiendi ijayo kwenye mchezo wa La Liga, Barcelona inaongoza msimamo wa La Liga mpaka sasa kwa alama 18 huku Real Madrid ikishika nafasi ya tano kwa alama 14.