
Lionel Messi akipewa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Chile
Mwamuzi wa mchezo huo, Mario Diaz de Vivar aliwatoa Lionel Messi na Gary Medel baada ya kukwaruzana uwanjani, kitendo ambacho Messi hakukifurahia na akisisitiza kuwa ulikuwa ni muendelezo wa mipango mibovu na upendeleo unaofanywa na Shirikisho la Soka la Amerika Kusini CONMEBOL.
Mchezo ulimalizika kwa Argentina kupata ushindi wa mabao 2-1, mabao yakifungwa na Paulo Dyabala na Sergio Aguero, huku bao pekee la Chile likifungwa na Arturo Vidal, lakini Messi hakuonekana wakati wa kupewa zawadi baada ya mchezo kumalizika.
"Hakuna shaka yoyote, mazingira yote haya yanatengenezwa kwa ajili ya kuwafaidisha Brazil na ninaamini VAR na hata waamuzi hawatokuwa sehemu ya maamuzi sahihi katika mchezo wa fainali", amesema Messi.
"Sitaki kuwa mmoja wa wahusika katika rushwa ya aina hii, hatukutakiwa kuwa katika uonevu huu ambao tumekutana nao katika Copa America ya mwaka huu. Tulipaswa tufike mbali katika mashindano lakini tulizuiwa tusifike fainali, rushwa, waamuzi na vingine vingi vimewanyima watu uhondo wa kushuhudia kandanda safi".
"Mimi mara zote nasema ukweli na ni muwazi, ndicho kinachonifanya kuwa mtulivu hivi", ameongeza Messi.
Michuano hiyo itamalizika leo kwa mchezo wa fainali kupigwa kati ya wenyeji Brazil na Peru.