Saturday , 24th May , 2014

Kukubalika kwa timu ya Mbeya City kumeleta changamoto kubwa katika ligi kuu bara msimu huu na kujizolea mashabiki kote nchini huku jezi za timu hiyo zenye rangi ya zambarau zikiuzwa kama njugu

Kikosi cha timu ngumu ya Mbeya city ambacho pamoja na ugeni katika ligi kimeleta changamoto kubwa na kushika nafasi ya tatu

Kocha mkuu wa timu ya Mbeya city ambayo hivi sasa iko nchini Sudan ikishiriki michuano ya Nile Basin inayoshirikisha vilabu vya ukanda wa Afrika Mashariki na kati chini ya CECAFA amesema ligi kuu msimu ujao itakua ngumu zaidi ya msimu huu.

Akizungumzia ligi iliyopita Mwambusi amesema timu nyingi zilionesha ushindani hasa baada ya timu ndogo kama Mbeya city kutoa changamoto na hivyo zikafanya hata timu zile ambazo awali zilionekana kusuasua kama Mgambo na nyinginezo kuamka na kuanza kutoa ushindani kwa timu nyingine hasa katika mzunguko wa pili.

Aidha Mwambusi ametolea mfano kwa kusema kuwa baada ya wao kuonekana kufanya vema katika mzunguko wa kwanza ndiyo ikawa kama wamejichongea kwani mzunguko wa pili ulikua mgumu mno kwao kwakua kila timu waliyokua wakikutana nayo ilicheza kwa nguvu na hata kwa kukamia ili waweze kuifunga timu hiyo.

Akimalizia Mwambusi amesema kwa hali hiyo anataraji msimu ujao wa ligi kuu bara 2014/2015 utakua na ushindani mkubwa kwani kila timu zitataka kufanya kama walivyofanya wao lakini akawakumbusha kuwa mafanikio ya timu yake ni mazoezi, umoja na ushirikiano na nidhamu kwa ujumla.