Kipa wa Simba SC, Peter Manyika jana amemaliza dakika 90 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa kwa mara ya pili mfululizo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi
Manyika aliyekuwa langoni SImba SC ikishinda 1-0 katika mchezo huo wa Kundi B jana usiku uwanja wa Amaan, Zanzibar sasa anafikisha jumla ya mechi 19 za kudaka bila kufungwa kati ya 37 alizocheza.
Na katika mechi zote 37, Manyika amefungwa mabao 29 tu huku akijiweka katika mazingira mazuri ya kuendelea kudaka na kwenye Nusu Fainali dhidi ya Mtibwa Sugar kesho, baada ya kutofungwa katika mechi mbili mfululizo.
Mtoto huyo wa kipa wa zamani wa Yanga SC, Manyika Peter alidaka katika sare ya 2-2 na Jamhuri ya Pemba mchezo wa kwanza wa Kundi A, kabla ya kurudi tena katika mchezo dhidi ya URA, timu yake ikishinda 1-0 sawa na jana dhidi ya JKU.
Kocha Muingereza, Dylan Kerr anaonekana kuanza kujenga tena imani na Manyika baada ya kuimarika kwa kiwango cha kipa huyo siku za karibuni.
Na tatizo kubwa lililoyumbisha kiwango cha Manyika siku za karibuni ni kipa huyo kutofanya mazoezi ipasavyo.
Kocha wa makipa, Mkenya Rama Salim alikuwa anamlalamikia Peter Manyika licha ya kuwa kipa bora kuliko wote kikosini, lakini uvivu wa mazoezi unamfanya asiwe katika kiwango kizuri.
Alisema Manyika ana mwili ambao akizembea mazoezi wiki moja tu anakuwa bonge – na ndiko alikoanza kuelekea siku za karibuni.
Lakini taratibu Manyika ameanza kurudi katika umbo zuri kiuchezaji baada ya kuongeza juhudi za mazoezi na sasa anaaminika tena, kiasi cha kumrudisha benchi kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast.
Bado Manyika ana kazi ya kufanya ili kuimarisha kiwango chake zaidi, hatimaye siyo tu kuendelea kuwa ‘Simba One’ bali kufufua na ndoto za siku moja kuwa kipa namba moja wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Manyika alisajiliwa msimu uliopita kama kipa wa kikosi cha pili na kipa wa tatu wa kikosi cha kwanza, lakini kuumia kwa wakati mmoja kwa waliokuwa makipa wa kwanza (Ivo Mapunda) na wa pili (Hussein Sharrif) wakati huo, kulimfanya aanze kudaka mapema.