Monday , 12th Sep , 2016

Timu ya Majimaji ya Mjini Songea imeitaka Bodi ya Ligi pamoja na Shirikisho la Soka nchini TFF kusikiliza ombi lao la uwekaji sawa wa ratiba ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ili kuweza kuokoa gharama za usafiri kutoka mkoa mmoja mpaka mkoa mwingine.

Meneja wa timu ya Majimaji FC Godfrey Mvula amesema, ratiba iliyopangwa kwa upande wao haiwaathiri katika mechi za ligi kuu lakini athari kubwa inakuja kwa upande wa hali ya uchumi kwa upande wa timu kwani TFF na bodi ya ligi ilitakiwa kuangalia kama timu ina mechi mkoa mmoja wenye timu zaidi ya moja basi wamalize mechi zote za mkoa huo ili kuweza kuokoa gharama wanazotumia katika safari.

Mvula amesema, kwa upande wa kikosi wanaendelea kukiandaa vizuri ili kuhakikisha mpaka wanaenda katika mapumziko ya mzunguko wa kwanza wanakuwa katika nafasi nzuri ya msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara.