Katika taarifa yake, Afisa habari wa shirikisho la soka nchini TFF, Baraka Kizuguto amesema, mfumo huo umetokana na marekebisho ya kanuni za FDL yaliyofanywa hivi karibuni na kamati ya utendaji ya ya Shirikisho la Soka nchini TFF katika kikao chake kilichofanyika mjini Zsnzibar.
Kizuguto amesema, timu ya kwanza katika kundi la ligi hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 12 mwaka huu itapanda kucheza ligi kuu kwa msimu wa 2016/2017 wakati timu itakayoshika nafasi ya mwisho katika kila kundi itashuka kucheza ligi daraja la pili SDL kwa msimu 2016/2017.
Kundi A linaundwa na timu za African Lyon FC (Dar es Salaam), Ashanti United SC (Dar es Salaam), Friends Rangers FC (Dar es Salaam), Kiluvya United FC (Pwani), Kinondoni Municipal Council FC (Dar es Salaam), Mji Mkuu FC (Dodoma), Polisi Dar es Salaam na Polisi Dodoma.
Timu zinazounda kundi B ni Burkina Faso FC (Morogoro), Kimondo SC (Mbeya), Kurugenzi Mafinga FC (Iringa), Lipuli FC (Iringa), Njombe Mji FC (Njombe), Polisi Morogoro na Ruvu Shooting (Pwani).
Kundi C ni Geita Gold SC (Geita), JKT Kanembwa FC (Kigoma), JKT Oljoro (Arusha), Mbao FC (Mwanza), Panone FC (Kilimanjaro), Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers (Tabora).