Tuesday , 7th Jun , 2016

Shirikisho la Soka Tanzania TFF kupitia Idara ya Ufundi, imetangaza kozi nne (4) za Leseni za Shirikisho la Soka Afrika CAF zinazotarajiwa kuanza Juni 20 mwaka huu katika Mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam.

Rais wa CAF, Issa Hayatou

Kwa Mkoa wa Mwanza, TFF itaendesha kozi ya leseni Daraja C ambapo kozi hiyo inatarajiwa kuanza Juni 20 hadi Julai 4, mwaka huu ambako baadhi ya washiriki 29 wamekwisha kujiandikisha ingawa bado kuna nafasi 11 ili kutimiza darasa la wanafunzi 40.

Sifa za watakaochukua kozi hiyo ni kuwa kuwa na cheti ngazi ya kati (intermediate) na umahiri (activeness).

Kozi hii pia imewapa nafasi wale wenye ndoto za kuwa makocha wa mpira wa miguu kuomba kusomea.

Kwa Jiji la Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, kozi hiyo inaratibiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TFF, Vedastus Rufano anayepatikana kwa na Mwalimu atakuwa Wilfred Kidao ambaye ni Mkufunzi wa ukocha anayetambuliwa na CAF.

Kozi nyingine ni ya leseni Daraja B ambayo itafanyika kuanzia Julai 1, hadi Julai 16, mwaka huu mkoani Morogoro ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Idara ya Ufundi ya TFF iliyoko Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kozi nyingine ya leseni Daraja B inaratibiwa jijini Dar es Salaam ambayo kuanzia Julai 1, hadi Julai 16, mwaka huu ambako washiriki wa kozi hiyo ni ya TFF makocha ambao tayari walifanya kozi ya FIFA-IOC iliyofanyika Oktoba, 2014 hivyo kwa sasa wanatakiwa kuthibitisha kushiriki kabla ya Juni 15, 2016 katika ofisi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi.

Nafasi pia zipo kwa washiriki wengine nje ya kundi la wale wa Oktoba, 2014 na kwamba sifa ni kuwa na Leseni Daraja C na awe amewahi kufanya kazi ya ukocha angalau kwa mwaka mmoja na zaidi.
Kadhalika kozi nyingine ji ya Leseni Daraja A ambayo itafanyika kuanzia Julai 17, 2016 hadi Julai 31, mwaka huu kwa hatua ya kwanza yaani Module 1 wakati Module 2 itafanyika Novemba, mwaka huu.

Wakufunzi wa kozi hiyo ya juu ni Makocha Salum Madadi na Sunday Kayuni, kabla ya CAF kumleta mtoa tathimini ya matokeo ya makocha hao kabla ya kutoa leseni ya daraja husika.

Washiriki wa kozi hiyo wanatarajiwa kuwa makocha wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwani msimu wa mwisho wa makocha wa Leseni Daraja B na C ni msimu wa 2016/2017.

Kuanzia msimu wa 2017/2018 hakuna kocha anayeruhusiwa kuongoza timu kwa kukaa kwenye benchi la ufundi kama hana sifa ya Daraja B na C ambapo msimu huu wa 2016/2017 ni nafasi ya mwisho kwa makocha wenye leseni madaraja ya chini kukaa au kuongoza timu zinazoshiriki Ligi kuu.