Monday , 15th Feb , 2016

Chama cha Kuogelea nchini TSA kimesema wanaimani kozi ya makocha wa mchezo huo iliyoanza hii leo itasaidia kuwaendeleza wachezaji wengi kutoka hapa nchini watakaoweza kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kimataifa.

Katibu Mkuu wa TSA Ramadhan Namkoveka amesema, kozi hiyo imehudhuriwa na washiriki 35 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mwanza, Arusha na kutoka visiwani ambapo Chuo Kikuu cha Zanzibar pamoja na chama cha kuogelea kutoka visiwani Zanzibar.

Namkoveka amesema, wamepata pia kocha kutoka Longido ambapo kwa upande wao ni furaha kwani hawakujua kama wana wanachama eneo hilo na wanafanya mpango kwa ajili ya kuweza kuendeleza eneo hilo liweze kufahamika zaidi nchini na nje ya nchi katika mchezo huo.

Namkoveka amesema, wamepata changamoto lakini wanaifanyia kazi kwani katika kozi ya makocha pia kulikuwa na washiriki ambao wanachukua kozi ya kuogelea lakini mpaka sasa amefika mmoja hivyo wanaamini wengine wataendelea kufika kwa ajili ya kuchukua mafunzo hayo.