Tuesday , 30th Dec , 2014

MICHUANO ya kombe la mapinduzi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari Mosi mpaka Januari 13 mwakani kwa kushirikisha timu mbalimbali kutoka Tanzania Bara, Uganda na wenyeji Zanzibar.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFA, Khasim Salum amesema ratiba ya michuano hiyo inatarajiwa kutoka kesho kutokana na baadhi ya timu alikwa kushindwa kuhakiki ushiriki wao mpaka sasa.

Salum amesema timu zote ambazo zimehakiki kushiriki michuano hiyo ambazo ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo KCC FC kutoka Uganda pamoja na timu kutoka Tanzania Bara ambazo ni Yanga Sc, Azam Fc, Simba Sc na Mtibwa Sugar zinatakiwa kuwasili visiwani humo Desemba 31 kwa ajili ya kuanza maandalizi.

Salu amesema, timu wenyeji wa michuano watawakilishwa na mabingwa wa Zanzibar KMKM, Police FC, JKU, Mtende Rangers na Shaba FC tayari zinaendelea na maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka nchini, Boniface Wambura amesema, Ligi kuu Tanzania Bara haitasimama isipokuwa timu nne zinazoshiriki michuano hiyo zitasimama kucheza ligi kuu Tanzania Bara katika mzunguko wa tisa na wa kumi ambapo zitacheza baada ya kumaliza michuano hiyo.