Tuesday , 17th Mar , 2015

Mwili wa aliyekuwa kocha msaidizi wa Timu ya Taifa, Taifa Stars umezikwa leo jijini Mwanza na familia baada ya kuwa na mgogoro kati ya Familia na Chama cha Mpira Mkoani Mwanza MZFA juu ya kuzika mwili wa Kocha Marsh.

Marsh alifariki dunia Jumamosi alfajiri baada ya kusumbuliwa na maradhi ya saratani ya koo ambapo alikwenda Muhimbili kuhudhuria kliniki ya kawaida ya ugonjwa wa saratani ya koo ambayo iligundulika alipolazwa awali hapo na kufanyiwa upasuaji na baadaye kuruhusiwa kurudi nyumbani kwake Mwanza.

Mwili wake uliagwa Jumapili mchana Hospitali ya Muhimbili, ambako walijitokeza mashabiki wa soka, makocha, wachezaji wa sasa na wa zamani ambapo miongoni mwa waliokuwepo ni makocha Charles Boniface Mkwasa aliyewahi kufanya naye kazi akiwa Twiga Stars, na Juma Pondamali aliyefanya kazi naye Taifa Stars.

Pia walikuwapo wachezaji wa Twiga Stars kumuaga kocha huyo ambaye mwili wake ulisafirishwa kwa njia ya barabara na amezikwa leo jijini Mwanza.

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ na mwaka 2006 alipandishwa timu ya wakubwa.

Ukiacha timu za Taifa, Marsh amewahi kufundisha klabu za Toto African ya Mwanza, 82 Rangers, Geita Gold Mines, Kagera Sugar ya Kagera na Azam FC ya Dar es Salaam na akiwa na Kagera Sugar mwaka 2004 alitwaa Kombe la Tusker akiwa na klabu hiyo ya Missenyi.