Monday , 1st Jul , 2019

Naibu Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Omar Kaya ametangaza rasmi kuwa ataondoka katika klabu hiyo kuanzia hii leo.

Picha ya wachezaji wa U20 na baadhi ya viongozi wa Yanga

Kaya ameamua kuondoka katika uongozi wa klabu hiyo baada ya kumalizika rasmi kwa mkataba wake ndani ya klabu ambapo kwa maamuzi yake ameomba kupumzika.

Akitangaza katika mkutano na waandishi wa habari, Omar Kaya amesema, "shukrani kwa viongozi walionitangulia kwa sababu haya mambo tunarithishana, leo yupo huyu na kesho anakuja huyu. Nitumie fursa hii pia kuweka vizuri maana nimeona asubuhi kumwekuwa na maneno mengi yakiandikwa kwenye mitandao ambayo siyo ya kweli".

"Sijamalizana na uongozi kwa matatizo au kufukuzana, ni kitu ambacho nliomba mwenyewe kwa ridhaaa yangu kwa heshima na taadhima kutokuongeza mkataba lakini tutaendelea kusaidiana kwa sababu wote tuko kwa ajili ya kujenga timu ya Yanga. Mimi nipo na wakinihitaji tutasaidiana kuijenga klabu yetu", ameongeza Kaya.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela amesema kuwa nafasi ya Omar Kaya kama Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga itashikiliwa na Afisa Habari wa klabu, Dismas Ten huku mchakato wa kuwapata viongozi wa kuziba nafasi mbalimbali ukiendelea.