Tuesday , 8th Sep , 2015

Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara msimu wa 2015/2016 inatazamiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi ya Septemba 12 kwa michezo saba kuchezwa katika viwanja tofauti nchini huku mchezo mmoja ukichezwa siku ya Jumapili uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Baraka Kizuguto amesema, timu ya Kagera Sugar inayotumia uwanja wa Kaitaba wa Mjini Bukoba itacheza michezo yake mitatu ya awali ya nyumbani katika mzunguko wa kwanza katika uwanja wa Al Hassan mwinyi wa mjini Tabora.

Kizuguto amesema, mechi hizo dhidi ya Toto Africans September 26, JKT Ruvu September 30, Tanzania Prisons Oktoba 4 na Yanga Oktoba 31 itachezwa Uwanja huo ili kupisha shughuli ya uwekaji nyasi bandia inayoendelea kwenye uwanja wao wa Kaitaba mjini Bukoba unaofanywa na wataalamu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mechi zitakazochezwa siku ya Jumamosi ni Ndanda FC ya Mtwara watakuwa wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nagwanda Sijaona mjini Mtwara, wana kimanumanu African Sports watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku wana Lizombe Majimaji wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Azam FC watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons katika uwanja wa Chamazi Complex, Stand United FC chama la wana watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumapili ligi kuu itaendelea kwa mchezo mmoja tu utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga SC watawakribisha wagosi wa kaya Coastal Union.